Pentecost – Swahili

French | German | Spanish | Swahili | Vietnamese
Matendo ya Mitume Mlango 2
- Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.
- Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.
- Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.
- Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.
- Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu.
- Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
- Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya?
- Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?
- Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia,
- Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu,
- Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.
- Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?
- Wengine walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya.
- Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu.
- Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana;
- lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli,
- Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto.
- Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri.
- Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi.
- Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo kuu na iliyo dhahiri.
- Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.
- Enyi waume wa Israeli, sikilizeni maneno haya: Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua;
- mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkamsulibisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua;
- ambaye Mungu alimfufua, akiufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao.
- Maana Daudi ataja habari zake, Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote, Kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike.
- Kwa hiyo moyo wangu ukapendezewa, ulimi wangu ukafurahi; Tena mwili wangu nao utakaa katika matumaini.
- Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; Wala hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu.
- Umenijuvisha njia za uzima; Utanijaza furaha kwa uso wako.
- Waume, ndugu zangu, mniwie radhi, niseme kwa ujasiri mbele yenu habari za baba yetu mkuu, Daudi, ya kuwa alifariki akazikwa, na kaburi lake liko kwetu hata leo.
- Basi kwa kuwa ni nabii, akijua ya kuwa Mungu amemwapia kwa kiapo, ya kwamba katika uzao wa viuno vyake atamketisha mmoja katika kiti chake cha enzi;
- yeye mwenyewe akitangulia kuyaona haya, alitaja habari za kufufuka kwake Kristo, ya kwamba roho yake haikuachwa kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu.
- Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake.
- Basi yeye, akiisha kupandishwa hata mkono wa kuume wa Mungu, na kupokea kwa Baba ile ahadi ya Roho Mtakatifu, amekimwaga kitu hiki mnachokiona sasa na kukisikia.
- Maana Daudi hakupanda mbinguni; bali yeye mwenyewe anasema, Bwana alimwambia Bwana wangu, Keti upande wa mkono wangu wa kuume.
- Hata nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.
- Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.
- Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
- Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
- Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.
- Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi.
- Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.
- Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.
- Kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na mitume.
- Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika,
- wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja.
- Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe,
- wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.
Source: WordProject
Holy Trinity Church